Kwa mujibu wa Mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Mashhad, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mustafa Rostami, Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu vya Nchini Iran, jana Jumatatu, tarehe 11 Aban, katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Kimataifa wa Wanamapambano Walio Ugenini, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Haram ya Imam Ridha (as), akisisitiza kwamba; mapambano dhidi ya ubeberu yana mizizi mirefu katika mafundisho ya Manabii wa Mwenyezi Mungu na maarifa ya Kiislamu, alisema: Kusimama imara mbele ya madhalimu na mabeberu ni mwenendo endelevu wa Manabii wa Mwenyezi Mungu na Mawalii wa dini. Njia hii, kupitia Mapinduzi ya Kiislamu na mwamko wa mataifa ya Kiislamu, imeingia katika hatua mpya.
Akizungumzia kufanyika Mkutano wa Kumi na Moja wa Kimataifa wa Wanamapambano Walio Ugenini, ambao umefanyika kwa kaulimbiu ya kuufahamu ubeberu na kupambana nao, alisema: Mkutano huu wa kitaaluma unafanyika kwa kushirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu, wanazuoni na walimu wa Hawza na vyuo vikuu. Katika mkutano huu, kunajadiliwa mada mbalimbali, zikiwemo uelewa wa ubeberu katika mfumo wa fikra wa Kiongozi Shahidi, uwekaji wa nyaraka za kisheria kuhusu jinai za wavamizi wa Marekani na Wazayuni katika eneo hili na katika vita vya hivi karibuni, ufuatiliaji wa kisheria wa jinai hizo, pamoja na uchunguzi wa uwezo wa jamii wa kustahimili changamoto, kwa kusisitiza nafasi na mchango wa wanawake.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu Nchini Iran aliongeza: Katika hafla ya kufunga mkutano huu pia, wawakilishi wa mataifa yenye msimamo wa kupinga ubeberu na wapambanaji walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubeberu watatambuliwa na kuheshimiwa katika jirani ya Haram tukufu ya Imam Ridha (as).
Mapambano dhidi ya ubeberu ni mwenendo endelevu wa Manabii wa Mwenyezi Mungu
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akieleza kwamba mapambano dhidi ya ubeberu yameendelea katika historia yote ya dini za Mwenyezi Mungu, alibainisha: Katika Qur’ani Tukufu, ujumbe wa Mtume Mtukufu (saww) na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), kuna mifano iliyo wazi ya namna Manabii na Mawalii wa Mwenyezi Mungu walivyosimama imara dhidi ya chuki, uhasama na dhuluma za watu wenye nia mbaya na mabeberu.
Akizungumzia mwenendo wa Imam Jawad (as) na nafasi yake tukufu miongoni mwa Waislamu, alisema: Imam Jawad (as) aliuawa kishahidi akiwa na umri wa miaka 25, ilhali alikuwa miongoni mwa shakhsia kubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata Waislamu ambao hawakuamini katika Uimamu wake walikuwa wakimpa nafasi ya kiroho na heshima ya pekee.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu, akizungumzia nafasi ya kihistoria ya mji wa Mashhad kama mahali alikouawa kishahidi na alipozikwa Imam Ridha (as), alisisitiza: Imam Ridha (as) na Maimamu wengine wa Ahlul-Bayt (as), katika kipindi cha maisha yao, walikabiliwa na chuki na uadui wa watawala wa Kitaghuti na mabeberu wa zama zao. Njia ya mapambano na kusimama imara dhidi ya mfumo wa utawala wa kibeberu iliendelea katika kipindi chote cha historia, mpaka pale ilipoingia katika hatua mpya kupitia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mwamko wa Waislamu duniani.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akiendelea na maelezo yake kuhusu msisitizo wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi juu ya suala la kudhoofika Marekani, alisema: Ayatullah Khamenei, tangu mwaka 1370 Hijria Shamsia, sambamba na kusambaratika Umoja wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti na kuanza kuundwa mfumo wa dunia wenye nguvu kuu moja, kinyume na mtazamo uliokuwa umezoeleka wakati huo, alizungumzia kuingia dunia katika kipindi cha mpito muhimu cha kihistoria na kutokea mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika muundo wa mgawanyo wa nguvu duniani.
Aliongeza: Katika mazingira ambayo, baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, ilidhaniwa kwamba dunia ilikuwa inaelekea katika mfumo wa utawala wa nguvu kuu moja na kwamba Marekani ingekuwa kama chifu wa kijiji cha dunia na kuwa na nguvu zisizokuwa na mpinzani, Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alitathmini kwamba mabadiliko yaliyokuwa yakisubiriwa yangekuwa tofauti na matarajio hayo, na akatoa taarifa kuhusu kubadilika mahusiano ya mgawanyo wa nguvu duniani.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu Nchini Iran, akizungumzia maelezo ya baadaye ya Kiongozi Shahidi kuhusu kipindi hicho muhimu cha mpito wa kihistoria, alisema: Katika miaka ya mwisho ya maisha yake matukufu pia, alisisitiza kwamba nguvu zilikuwa zikihamishwa kutoka Magharibi kwenda Mashariki, kwamba Marekani ingetengwa katika mabadiliko mapya, na kwamba mkondo wa fikra wa Muqawama, ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauwakilisha, ungekuwa mkondo mkuu wa fikra miongoni mwa mataifa.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akizungumzia mabadiliko yaliyotokea katika vita vya Ukraine, alisema: Katika mwezi wa kwanza kabisa tangu kuanza kwa vita hivyo, Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, kupitia ujumbe aliouelekeza kwa wanafunzi wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi nchini Ulaya, alizichukulia harakati za kisiasa na kijeshi zilizokuwa zikiendelea kuwa sehemu ya kipindi kilekile muhimu cha mpito wa kihistoria ambacho hapo awali alikuwa amekizungumzia.
Aliendelea kusema: Katika ujumbe huo, alisisitiza umuhimu wa kutambua makundi na misimamo mbalimbali katika kipindi cha muda mfupi, pamoja na nafasi ya vijana katika kuhakikisha ushindi wa upande wa haki katika kipindi cha muda wa kati. Mtazamo wa aina hii ulidhihirisha kwamba Kiongozi Shahidi, kwa kuwa na uelewa sahihi wa mabadiliko ya dunia, alikuwa amezingatia umuhimu wa kizazi cha vijana kushiriki kikamilifu katika masuala na mikondo ya matukio yaliyokuwa yakisubiriwa.
Mkuu huyo wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu alisisitiza: Uchambuzi wa Kiongozi Shahidi kuhusu kudhoofika mfumo wa utawala wa kibeberu na kuundwa kwa mfumo mpya wa mgawanyo wa nguvu duniani ulijengwa, kwa upande mmoja, juu ya imani yake ya kina katika mafundisho ya Qur’ani Tukufu na maarifa ya Mwenyezi Mungu, na kwa upande mwingine, juu ya uelewa wake sahihi wa mabadiliko ya kisiasa na kimataifa.
Kiongozi Shahidi alibainisha njia huru ya Muqawama mbele ya mgawanyo wa pande mbili uliowekwa na Marekani
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akizungumzia misimamo ya Serikali ya Marekani baada ya tukio la Septemba 11 na kauli mbiu ya mgawanyo wa pande mbili ya George W. Bush, aliyesema “Yuko pamoja nasi au yuko dhidi yetu”, alisema: Rais wa wakati huo wa Marekani alitangaza kwamba mataifa yote duniani yalipaswa kusimama upande wa Marekani; vinginevyo, yangekuwa katika upande unaoipinga nchi hiyo na kuhesabiwa miongoni mwa waungaji mkono wa ugaidi.
Aliongeza: Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, akijibu mgawanyo huo wa pande mbili, alieleza wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiko upande wa magaidi wala haiambatani na Marekani, kwa sababu Marekani yenyewe ni miongoni mwa sababu kuu za kuibuka na kuungwa mkono kwa ugaidi.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu, alisisitiza: Kiongozi Shahidi, kwa kuweka wazi mpaka kati ya upande wa haki na mfumo wa utawala wa kibeberu, alibuni na kuongoza njia huru ya kusimama imara na kufanya Muqawama; njia ambayo leo athari zake zinaonekana katika mabadiliko ya kikanda na kimataifa.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akizungumzia vita vya hivi karibuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: Vita hivi havikuwa tu makabiliano kati ya Iran na Marekani au utawala wa Kizayuni, ambao ni mkono wa kijeshi na kikanda wa Marekani, bali mfumo mzima wa utawala wa kibeberu ulishiriki katika makabiliano hayo.
Akizungumzia kauli ya Katibu Mkuu wa NATO kuhusu kufanyika safari elfu tano za ndege za kivita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Ulaya pamoja na Marekani, alisema: Nchi kama Uingereza, Ufaransa, Italia na Ujerumani zilisogea upande wa Marekani, na katika vita hivi, taifa la Iran lilisimama imara dhidi ya mfumo mzima wa utawala wa kibeberu.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu, aliendelea kusema: Katika uwanja huu wa mapambano, mataifa yaliyo huru yalisimama upande wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; kuanzia taifa shujaa na lenye msimamo thabiti la Yemen, wapiganaji wa Lebanon na Palestina, hadi vikosi vya Muqawama nchini Iraq. Hata hivyo, upande wa pili, mfumo mzima wa utawala wa kibeberu ulisimama dhidi ya utashi wa taifa la Iran.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akizungumzia matokeo ya vita vya hivi karibuni na mabadiliko ya hali ya eneo hili, alisema: Kilichotokea katika makabiliano hayo ni kushindwa na kudhalilishwa mfumo wa utawala wa kibeberu, pamoja na kufichukamipaka ya nguvu za Marekani.
Akizungumzia kauli za David Petraeus, Mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Kamanda wa zamani wa Jeshi la Marekani nchini Iraq, kuhusu hali ya kambi za kijeshi za nchi hiyo katika eneo hili, alisema: Petraeus ametangaza kwamba kambi zote za kijeshi za Marekani katika eneo hili zimekuwa zisizoweza kutumika. Kukiri huku kumetolewa na mtu ambaye katika historia yake amewahi kuwa kamanda wa kijeshi na Mkuu wa Shirika la CIA, na ambaye ana ufahamu kuhusu masuala ya kimkakati ya Marekani.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu aliongeza: Mabadiliko ya mizani ya nguvu hayajabaki katika uchambuzi wa maafisa na wanafikra walio nje ya Marekani pekee, bali hata ndani ya nchi hiyo yametolewa maoni kuhusu kuongezeka nguvu na nafasi ya Iran katika eneo hili.
Akizungumzia kauli za Barack Obama, Rais wa zamani wa Marekani, kuhusu nafasi ya Iran katika mabadiliko ya eneo la Mlango-Bahari wa Hormuz na ushawishi wake katika soko la mafuta duniani, alisisitiza: Leo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefikia nafasi ambayo inatekeleza jukumu lenye ushawishi wa kuamua katika mizani ya kimkakati ya eneo hili na dunia.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akizungumzia mojawapo ya utabiri wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi kuhusu kubadilika nafasi ya Iran katika mizani ya kimataifa, alisema: Ayatullah Khamenei alikuwa amesisitiza hapo awali kwamba; siku itafika ambapo taifa la Iran litazichambua na kuzitathmini nguvu za Magharibi kutokana na jinai zake. Leo, dalili za kutimia kwa mtazamo huu zimejitokeza wazi katika mabadiliko ya kimataifa.
Alisisitiza: Leo, wapiganaji na vikosi vya Muqawama katika Mlango-Bahari wa Hormuz wanaathiri mizani ya kimkakati na kiuchumi ya dunia. Aidha, mataifa yaliyo huru katika maeneo mbalimbali ya dunia, yakiwemo mataifa ya Afrika na miji ya Ulaya kama Paris na Roma, yanaitikia sera za mfumo wa utawala wa kibeberu kwa kujitokeza na kufanya maandamano.
Mkuu wa Taasisi ya Uwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu, akisisitiza umuhimu wa kuyageuza mafanikio ya mkondo wa Muqawama kuwa utamaduni mpana wa kimataifa, alisema: Heshima na nguvu ambazo mkondo wa Muqawama na wapambanaji dhidi ya ubeberu wamezianzisha, zinapaswa kugeuzwa kuwa utamaduni wa jumla wa jamii, ili mataifa yaliyo huru duniani nayo yaungane na mkondo huu.
Umuhimu wa kueleza kwa misingi ya kitaaluma mafanikio ya Jihadi ya Muqawama duniani
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rostami, akisisitiza umuhimu wa kuandaa vikao maalumu vya kitaaluma na kufanya tafiti za kisayansi katika uwanja wa kuufahamu ubeberu na kupambana nao, alisema: Makala, tafiti na vikao vya kitaaluma vya mkutano huu vinaweza kutekeleza nafasi yenye ufanisi katika kueleza kwa usahihi zaidi asili ya mfumo wa utawala wa kibeberu na mafanikio ya Jihadi ya Muqawama.
Maoni yako